Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Mh. Dr. Marry M. Mwanjelwa (mb) Atembelea Wakala ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA)

Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Dkt. Mary Mwanyelwa (MB) ametembelea ofisi za TaGLA jijini Dar es Salaam ili kujionea shughuli, huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na Wakala.

Akimkaribisha Naibu Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Nd. Charles Y. Senkondo alimueleza historia fupi ya kuanzishwa kwa Wakala na huduma zitolewazo na Wakala ikiwemo huduma ya Mtandao kwa Njia ya Video (Video Conference), vile vile Naibu Waziri alipata fursa ya kuongea na watumishi wa Wakala na kutembelea idara za Wakala ili kujionea jinsi wanavyofanya kazi. Akiwa katika ofisi za TaGLA Mh. Dkt Mwanjelwa alipata fursa ya kuongea mubashara na watumishi wa Utumishi waliopo makao makuu jijini Dodoma akiwa kwenye kumbi za TaGLA, Dar es Salaam. Pia akiwa kumbiza TaGLA Dar es Salaam aliweza kuwasiliana na Chuo cha Serikali cha Kenya (Kenya School of Government) , Nairobi kwa kutumia mawasiliano ya mtandao wa njia ya video (Video Conference).

Naibu Waziri Mh. Dkt Mary Mwanjelwa alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji pamoja na watumishi wote wa TaGLA kwa mapokezi mazuri na kusema ziara hiyo imekuwa sehemu ya kujifunza mambo mengi ikiwemo jinsi ya kutumia teknolojia katika kubadilishana ujuzi na kufanya mafunzo kwa mtandao, na jinsi gani Serikali imeweza kuokoa fedha nyingi kwa kutumia huduma za Wakala. Vile vile Mh. Naibu Waziri aliwaagiza TaGLA waongeze juhudi ya kujitangaza na kuwa wabunifu kuwavutia watumiaji  ili Watanzania wengi wafaidike na huduma nzuri za Wakala.

Naibu Waziri aliwaasa watumishi wa TaGLA kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa ili kuongeza tija na kuongeza ufanisi katika majukumu yao na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano (5).

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.