Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

Naibu Katibu Mkuu Utumishi afunga mafunzo ya Mfumo wa Taarifa za Usimamizi na malipo ya mishahara ya Watumishi wa Umma (HCMIS) katika ofisi za TaGLA jijini Dar es Salaam

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) kwa kushirikiana na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kuendesha mafunzo ya Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Watumishi wa Umma (HCMIS) katika ofisi zake  jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo ya wiki mbili yalishirikisha maafisa rasilimali watu kutoka taasisi mbalimbali za umma, baada ya mafunzo hayo washiriki walikabidhiwa vyeti vya ushiriki na Naibu Katibu Mkuu kutoka utumishi, Dkt Francis Michael.

Akifunga mafunzo hayo ya wiki mbili, naibu katibu mkuu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Francis Michael aliwapongeza TaGLA kwa kuratibu mafunzo hayo kwa ufanisi na aliwataka washiriki wa mafunzo kuzingatia yale yote waliyofundishwa na wakawe watumishi wa mfano watakaporudi sehemu zao za kazi na wakawe viungo wazuri baina mwajiri na watumishi, na alisema serikali haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu afisa rasilimali watu yoyote atakaye kiuka maadili ya utumishi wa umma.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na wakufunzi kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na TaGLA, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo maafisa rasilimali watu katika sekta ya Umma ili wawe na uwezo wa kuuelewa na kuutumia kwa ufanisi Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Watumishi wa Umma (HCMIS) kwa kuhakikisha watumishi wapya serikalini wanaingizwa kwenye mfumo wa mshahara serikalini (payroll) kwa usahihi na kwa wakati, kuwawezesha waajiri na maafisa rasilimali watu na serikali kwa ujumla kuingiza taarifa za watumishi kwa usahihi katika mfumo wa malipo ili kusaidia katika kufanya maamuzi yenye tija, kuhakikisha mabadiliko ya mishahara kwa watumishi wa Umma yanafanyika kwa usahihi na kwa wakati, kuondoa urasimu wa kulipa tofauti ya mshahara wa mtumishi wa Umma (salary areas) na kuondoa tatizo la watumishi hewa (ghost workers) katika Utumishi wa Umma. Mafunzo hayo ya wiki mbili yaliendeshwa katika maabara ya kisasa  ya kompyuta iliyopo katika ofisi za TaGLA jijini Dar es Salaam na kila mshiriki alitumia kompyuta moja kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.