Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TAGLA YAENDESHA MAFUNZO YA MAISHA BAADA YA KUSTAAFU KAZI KWA WATUMISHI MJINI MOROGORO

TaGLA imeendesha mafunzo ya siku tano kwa watumishi walio katika ajira rasmi  mjini Morogoro. Warsha hiyo ya siku tano inashirikisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali hapa nchini. Baada ya warsha hiyo washiriki walikabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Akitoa mafunzo hayo, mkufunzi  kiongozi Nd. Anselm Namala alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa washiriki maarifa, mbinu na uzoefu wa jinsi ya kujiandaa vema na maisha baada ya kustaafu, kwani tafiti zimebaini kuwa wastaafu wengi hukumbwa na misukosuko ya kifedha, kiafya na kimaisha kwa ujumla. Moja kati ya sababu kubwa ya wastaafu kukumbwa na misukosuko hiyo na kushindwa kuihimili vema maisha ni kutokuwa na mipango madhubuti ya maisha baada ya kustaafu kazi.

 Mafunzo ya Kujiandaa na Maisha Baada ya Kustaafu Kazi yanalenga kumwezesha mfanyakazi kuanza kujiandaa kisaikolojia juu ya maisha baada ya kustaafu, kutoa elimu juu ya kuandaa mpango binafsi wa kustaafu, kutoa mbinu za kijasiriamali na stadi za maisha na kutoa elimu ya afya. Mafunzo hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kubadilishana ufahamu na uzoefu kutokana na mazingira watokayo, vilevile washiriki walipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya binafsi iliyofanikiwa kwa ajili ya kujionea uhalisia wa mafunzo hayo.

TaGLA inatoa wito kwa wadau kutembelea tovuti ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma zitolewazo na wakala.