Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

MADAKTARI WA MAGONJWA YA MOYO WAPATA MAFUNZO YA UZIBUAJI WA VALVU YA MOYO KWA NJIA YA MTANDAO KUTOKA NCHINI INDIA

Wakala ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA) imeendesha mdahalo juu  ya uzibuaji valvu ya Moyo ikishirikiana na Hospitali ya Continental ya nchini India ili kubadilishana uzoefu na wataalam wa nchini. Mdahalo huu uliendeshwa kwa masafa kutumia teknolojia ya videoconference.

Akizungumza katika mafunzo hayo ya uzibuaji wa Valvu ya Moyo Mkurugenzi Mtendaji wa wakala hiyo Charles Senkondo amesema kuwa katika mkutano huo watalaam wamepata uzoefu kutoka kwa Mkuu wa Cath Lab ya Hospitali ya Continental ya nchini India Profesa Bharath Purohit. Senkondo amesema kuwa tangu kuanza kwa midahalo kwa njia ya Mtandao kada mbalimbali zimepata mafunzo katika Mada zinazoandaliwa na taasisi zilizopo mbara ya Amerika, Ulaya na Asia kwa kushirikiana na wakala ya Mafunzo kwa njia ya Mtandao, TaGLA. Amesema wakala hiyo ndio inaongoza kwa nchi za Afrika katika uendeshaji wa midahalo na mafunzo kwa masafa.

Aidha amesema kuwa eneo hilo la uzibuaji valvu ya Moyo umekuwa na mwitikio mkubwa kwa upande wa madaktari wetu katika kupata uzoefu wa Hospitali ya Continental ya nchini India. Daktari Bingwa wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI 
Dr. Tatizo Waane amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika Sekta ya Afya kwa watalaam kupata ujuzi zaidi kutoka kwa wabobezi wa masuala ya magonjwa ya moyo na pia mafunzo hayo yanapunguza hata gharama za matibabu kwakuwa wataalamu wengi wanapopata mafunzo wanapata uzoefu na kufanya kazi nzuri ya kutibu magonjwa hayo hapahapa nyumbani.

Dr. Tatizo Waane ameongeza kuwa kuna kila sababu ya kuwa na mipango mahsusi ili kupata midahalo kama hii yenye manufaa kwa kada zote jambo ambalo litawezesha wataalam wa hapa nchini kupata weledi wa namna ya kukabili magonjwa ya moyo.

Kwa upande wa TaGLA, Senkondo ametoa wito kwa Watanzania kutumia huduma zinazotolewa na Wakala ili kuongeza ufahamu, kuongeza ubunifu na weledi ili kwenda sambamba na kasi ya kujenga taifa lenye uwezo wa kustahimili kujenga uchumi wa viwanda unaohitaji kujenga tabia ya kujijengea uwezo katika taasisi zatu za umma na sekta binafsi.