Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TaGLA YAVUTIA WENGI MAONESHO YA TATU YA BIDHAA ZA VIWANDA NCHINI KATIKA UWANJA WA MWL. JULIUS K. NYERERE

TaGLA imeshiriki katika maonesho ya tatu ya viwanda nchini katika uwanja wa Mwl Julius K. Nyerere na kuvutia wadau wengi walioshiki na kutembelea maonesho hayo.

TaGLA imekuwa ikiwajengea uwezo wadau nchini kwa kuwapatia mafunzo na semina kwa kutumia wakufunzi mahiri na waliobobea wa ndani na nje ya nchi. Pamoja na mafunzo, Wakala inatoa jukwaa la mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) na kwa kuwa kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ni kukuza uchumi wa viwanda, Wakala ina nia kuwezesha utumizi wa mawasiliano kwa wawekezaji. Wakala katika maonesho hayo ilielimisha na kuwashauri wadau umuhimu wa mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video na jinsi gani mtandao huo unavyoweza kuchangia katika kukuza uchumi wa viwanda kwa wawekezaji mmoja mmoja na pia kuwaunganisha na kliniki za Biashara.

Akifungua maonesho hayo ya tatu ya viwanda nchini naibu waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Mhandisi Stella M. Manyanya, akiwa katika banda la TaGLA alitoa pongezi kwa kuwajengea uwezo wadau na kuitangaza huduma ya mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) katika maonesho hayo. Aliwaagiza kwa nafasi iliyopo huduma ya mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) itumike pia kuwawezesha wenye viwanda kuongeza ufanisi na tija kwani huduma hiyo ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, kuwakutanisha wadau wengi kwa wakati mmoja, maamuzi kufanyika kwa wakati, kuepukana na ajali za barabarani na kuongeza kasi ya uwekezaji kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Ndg. Charles Senkondo alimshukuru naibu waziri kwa ufunguzi wa maonesho na kutembelea banda la TaGLA na kuahidi kutoa ushirikiano katika kukuza matumizi ya mtandao wa mawasiliano wa njia ya video (Video Conference) ili kufikia malengo ya kuwa na uchumi imara wa viwanda nchini.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma zitolewazo na wakala.