Wasiliana Nasi: info@tagla.go.tz | +255 22 2123705 / +255 22 2123709 / +255 22 223711

TaGLA imeshiriki katika maonesho ya tatu ya viwanda nchini katika uwanja wa Mwl Julius K. Nyerere na kuvutia wadau wengi walioshiki na kutembelea maonesho hayo.

TaGLA imekuwa ikiwajengea uwezo wadau nchini kwa kuwapatia mafunzo na semina kwa kutumia wakufunzi mahiri na waliobobea wa ndani na nje ya nchi. Pamoja na mafunzo, Wakala inatoa jukwaa la mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) na kwa kuwa kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ni kukuza uchumi wa viwanda, Wakala ina nia kuwezesha utumizi wa mawasiliano kwa wawekezaji. Wakala katika maonesho hayo ilielimisha na kuwashauri wadau umuhimu wa mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video na jinsi gani mtandao huo unavyoweza kuchangia katika kukuza uchumi wa viwanda kwa wawekezaji mmoja mmoja na pia kuwaunganisha na kliniki za Biashara.

Akifungua maonesho hayo ya tatu ya viwanda nchini naibu waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Mhandisi Stella M. Manyanya, akiwa katika banda la TaGLA alitoa pongezi kwa kuwajengea uwezo wadau na kuitangaza huduma ya mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) katika maonesho hayo. Aliwaagiza kwa nafasi iliyopo huduma ya mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) itumike pia kuwawezesha wenye viwanda kuongeza ufanisi na tija kwani huduma hiyo ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, kuwakutanisha wadau wengi kwa wakati mmoja, maamuzi kufanyika kwa wakati, kuepukana na ajali za barabarani na kuongeza kasi ya uwekezaji kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Ndg. Charles Senkondo alimshukuru naibu waziri kwa ufunguzi wa maonesho na kutembelea banda la TaGLA na kuahidi kutoa ushirikiano katika kukuza matumizi ya mtandao wa mawasiliano wa njia ya video (Video Conference) ili kufikia malengo ya kuwa na uchumi imara wa viwanda nchini.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma zitolewazo na wakala.

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) kwa kushirikiana na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yaendelea kuendesha mafunzo ya Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Watumishi wa Umma (LAWSON) katika ofisi za TaGLA  jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo ya wiki mbili yanashirikisha maafisa rasilimali watu kutoka taasisi mbalimbali za umma, baada ya mafunzo hayo washiriki watakabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Mafunzo hayo yataendeshwa na wakufunzi kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na TaGLA, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo maafisa rasilimali watu katika sekta ya Umma ili wawe na uwezo wa kuuelewa na kuutumia kwa ufanisi Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Watumishi wa Umma (LAWSON) kwa kuhakikisha watumishi wapya serikalini wanaingizwa kwenye mfumo wa mshahara serikalini (payroll) kwa usahihi na kwa wakati, kuwawezesha waajiri na maafisa rasilimali watu na serikali kwa ujumla kuingiza taarifa za watumishi kwa usahihi katika mfumo wa malipo ili kusaidia katika kufanya maamuzi yenye tija, kuhakikisha mabadiliko ya mishahara kwa watumishi wa Umma yanafanyika kwa usahihi na kwa wakati, kuondoa urasimu wa kulipa tofauti ya mshahara wa mtumishi wa Umma (salary areas) na kuondoa tatizo la watumishi hewa (ghost workers) katika Utumishi wa Umma. Mafunzo hayo ya wiki mbili yataendeshwa katika maabara ya kisasa  ya kompyuta iliyopo katika ofisi za TaGLA jijini Dar es Salaam na kila mshiriki atatumia kompyuta moja kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo jinsi mfumo wa huo wa LAWSON unavyofanya kazi.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

Wakala ya Mafunzo kwa  Njia ya Mtandao Tanzania (TaGLA) yapokea ugeni kutoka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Idara ya TEHAMA mradi wa Serikali Mtandao kutoka nchini Lesotho. Ujumbe huo uliongozwa na Nd. Khiba Masiu ambaye ni mratibu wa mradi huo.

Akiwakaribisha wageni hao mbele ya watumishi wa TaGLA, Mkurugenzi Mtendaji wa TaGLA Nd. Charles Y. Senkondo alisema dhumuni kubwa la ujumbe huo ni kujifunza na kupata uzoefu kutoka TaGLA kwa kuwa Wakala imekuwa ikifanya vizuri  na kuwa kiungo bora kwa kuunganisha wanachama wa Mtandao wa Vituo vya Maendeleo barani Afrika (AADLC, www.aadlc.net) unaojumuisha nchi za Benin, Cote d’ Ivore, Kenya, Mali, Senegal, Tanzania na Uganda.

Kiongozi wa ujumbe huo Nd. Masiu aliwashukuru Watumishi wa TaGLA kwa mapokezi mazuri na aliendelea kusema ziara hiyo imekuwa sehemu ya kujifunza mambo mengi  ikiwemo jinsi ya kutumia teknolojia katika kubadilishana ujuzi na kufanya mafunzo kwa mtandao, na jinsi gani wanaweza kuanzisha wakala kama TaGLA nchini kwao.

Pamoja na kutembelea TaGLA, menejimenti ya TaGLA iliwawezesha wageni hao kujionea jinsi huduma ya Mawasiliano kwa njia ya Mtandao wa Video (Video Conference) unavyofanya kazi kwa kuwaunganisha kwenye mkutano wa moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Utumishi jijini Dodoma , kuwaunganisha na vituo vingine vya AADLC kutoka nchini Kenya, Uganda na Mali, na walipata fursa ya kutembelea taasisi nyingine ambazo tunashirikiana na TaGLA.

Akifafanua faida walizoziona kwa kuwa na taasisi kama TaGLA ni pamoja na kuweza kuwa na mafunzo ya moja kwa moja yanayofikia walengwa wengi kwa gharama nafuu, kuweza kupata wataalam waliobobea katika fani muhimu za kiutumishi kokote duniani, kutumia teknolojia ya videoconference kwa ajili ya kufanya maamuzi jumuishi kwa wakati na hivyo kuchangia kuboresha utumishi wa umma ili kutoa huduma bora zinazihotajika.

Wakala ya mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) yaendesha mafunzo ya siku tano ya huduma bora kwa wateja mjini Morogoro. Mafunzo hayo yanashirikisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali, baada ya kozi hiyo washiriki watakabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Mkufunzi mkuu wa kozi hiyo Dkt. Yustin Bangi alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha washiriki jinsi ya kuwahudumia wateja wakorofi, kujiamini kwenye maongezi ya simu, jinsi ya kuvutia wateja wapya na kuwaridhisha wateja waliopo ili waendelee kutumia huduma za taasisi husika. Vilevile kuwawezesha na kuwajengea washiriki uwezo zaidi wa kiutendaji na kuwaongeza ufanisi katika kuhudumia wateja kwa kutoa huduma bora ili kutimiza malengo na majukumu yao na vile vile kuendana na kasi ya sasa ya ukuaji wa uchumi na mapinduzi ya viwanda.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

TaGLA ni mwanachama wa Mtandao wa Vituo vya Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika (AADLC). AADLC ina jukumu la kuwawezesha watoa maamuzi na wataalamu pamoja na watendaji kupata na kushirikishana uzoefu na ujuzi uliopo duniani  kupitia mifumo ya mawasiliano kwa njia ya mtandao.

Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) inaiwakilisha Tanzania kwenye kongamano la kimataifa la Elimu Masafa barani Afrika  linalofanyika jijini Kigali nchini Rwanda.

Akifungua kongamano hilo mwenyekiti wa AADLC Ndg. Aliuo Mohamedi kutoka Mali alisema kongamano hilo linashirikisha vituo vya  Mtandao wa Mafunzo ya Maendeleo barani Afrika kutoka nchi mbalimbali.  Pamoja na ajenda kuu ya elimu masafa washiriki  pia walijadiliana masuala mbalimbali ya mtandao wao kwa lengo la kuuboresha mtandao huo ili ulete mageuzi na mapinduzi ya mawasiliano ya kiteknolojia barani Afrika, vile vile washiriki walibadilishana uzoefu, kwa mfano Dkt. Nfuka alifafanua jinsi TEHAMA  inavyotumika kama nyenzo wezeshi kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa Mfumo wa Ujifunzaji Kielektroniki (MUKI) kwenye  kutoa  mafunzo ya madiwani kwa njia ya elimu masafa nchini Tanzania ukizingatia vifaa walivyonavyo madiwani kwa kutumia simu zao za kiganjani kufanya  kila kitu: kusoma, kuangalia video, kutafakari, kufanya mazoezi, majadiliano, soga, kufanya mitihani na tathmini.

Nchi zinazoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Benin, Mali, Uganda, Kenya, Tanzania na Ivory Coast.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

Wakala ya mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA) yaendesha mafunzo ya siku tano kwa watumishi mbalimbali walio katika ajira rasmi  mjini Mrogoro. Warsha hiyo ya siku tano imeshirikisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali nchini, baada ya warsha hiyo washiriki walikabidhiwa vyeti vya ushiriki.

Akitoa mafunzo hayo, mkufunzi Nd. Anselm Namala alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa washiriki maarifa, mbinu na uzoefu wa jinsi ya kujiandaa vema na maisha baada ya kustaafu, kwani tafiti mbalimbali zimebaini kuwa wastaafu wengi hukumbwa na misukosuko mingi ya kifedha, kiafya na kimaisha kwa ujumla. Moja kati ya sababu kubwa ya wastaafu kukumbwa na misukosuko hiyo na kushindwa kuihimili vema ni kutokuwa na mipango madhubuti ya maisha baada ya kustaafu kazi.

Mafunzo ya Kujiandaa na Maisha Baada ya Kustaafu Kazi yamelenga kumwezesha mfanyakazi kuanza kujiandaa kisaikolojia juu ya maisha baada ya kustaafu, kuwaelimisha juu ya kuandaa mpango binafsi wa kustaafu, kuwapa mbinu za kijasiriamali na stadi za maisha na kutoa elimu ya afya. Mafunzo hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kubadilishana ufahamu na uzoefu kutokana na mazingira watokayo lakini pia walipata fursa ya kutembelea miradi ya ufugaji wa kuku na samaki.

TaGLA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti yetu ya www.tagla.go.tz ili kujua mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na wakala.

Matumizi jumuishi ya TEHAMA huleta ufanisi katika kufikia malengo na kuweka mifumo ya majiji endelevu duniani, ikiwemo Tanzania. Hii ilibainika kupitia mada iliyowasilishwa na Dkt. Hee-Su Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini kupitia mtandao wa videoconference, akitoa uzoefu wa nchini Korea Kusini juu ya jukwaa jipya na mapinduzi ya nne ya viwanda katika  kuleta maendeleo endelevu ya majiji  nchini Korea Kusini. Pamoja na mambo mengine , washiriki walibadilishana uzoefu na kuuliza maswali kuhusu mikakati ya kukuza majiji na kuleta mapinduzi ya viwanda ili  kufikia maendeleo endelevu katika majiji.

Baada ya semina hiyo washiriki wa Tanzania wakiongozwa na mkurugenzi mtendaji wa TaGLA, Nd. Charles Senkondo walibadilishana uzoefu  kwa kuchangia mawazo na hatua zipi zichukuliwe ili kutatua changamoto za miji na majiji yetu kwa kuiga mfano wa Korea Kusini ili isaidie ukuaji wa majiji yetu na kuleta mapinduzi ya viwanda. Washiriki waliona ipo haja ya kuandaa jukwaa la kitaifa na kuwashirikisha wadau kutoka sekta muhimu nchini ili kujadili suala la ukuaji wa miji na mapinduzi ya viwanda.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Majji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi mfululizo mwaka huu.

Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini.

Wito unatolewa kwa watanzania kutumia fursa hii ili kupata fursa ya kubadilishana mawazo na kubuni mbinu mpya za kuiwezesha Tanzania kuwa na majiji endelevu ya mfano kuweza kuiweka katika utayari wa kuwa nchi ya viwanda.

TaGLA imeendelea kuiwakilisha vyema Tanzania na bara la Afrika katika kushiriki Semina za Majiji Endelevu zilizoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo nchini Korea Kusini kwa Njia ya Mtandao wa Mawasiliano ya Video (Video Conference).

Mada iliyowasilishwa na Jin Hwa Kim kutoka Chuo cha Maendelo cha Korea jijini Seoul, Korea ya Kusini ilitoa uzoefu wa kutoka nchini Korea Kusini katika kukuza majiji ya kiutawala ili kuleta maendeleo  kutokana na uzoefu wa Korea Kusini kuanzisha jiji la kiutawala la Sejong. Katika mjadala huu, maandalizi mahsusi yalifanyika kuhakikisha mazingira bora ya kuishi na kufanya kazi yanaendelezwa, huduma za kijamii zinaandaliwa na kutolewa katika kanda maalum za jiji na hatua maalum zinachukuliwa ili taasisi za elimu zianzishe matawi ya kuhudumia watumishi na familia zao.

Washiriki wa Tanzania kutoka Halmashauri za Majiji, sekta binafsi, mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za elimu walishiriki kwa kuchangia uzoefu katika kutatua changamoto za majiji ya nchi zinazoendelea na kupata mrejesho kutoka Korea na nchi nyingine.

Semina hii ni muendelezo wa semina za Miji Endelevu, na  zitakuwepo kwa vipindi vingine vitatu kati ya sasa na Oktoba 2018, ikijumuisha tarehe 11 Septemba, tarehe 18 Septemba na tarehe 11 Oktoba 2018.

 Nchi zinazoshiriki katika semina hii ni pamoja na China, Vietnam, Philippines, Indonesia, Thailand, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, India, Tanzania na Korea Kusini. Washirki kutoka nchi hizo walipata wasaa wa kuuliza maswali na maswali yao yalijibiwa mubashara na mtoa mada kutoka  Korea Kusini kupitia njia ya mtandao wa mawasiliano ya video.